
Angel Wariael, binti aliyejeruhiwa Oktoba 29, afariki dunia Muhimbili Dar es Salaam. Angel Wariael,13, binti aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na kujeruhiwa na risasi kwenye matukio ya Oktoba 29 akiwa nyumbani kwao Manzese amefariki dunia. Hospitali imethibitisha kifo chake leo Novemba 18, 2026, kupitia Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Irene Charles Mbonde, pamoja na taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia. Katika taarifa kwa waandishi wa habari, Hospitali ya Taifa Muhimbili, (MNH) imetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huo, ikiwaombea nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu. Oktoba 31, 2026, The Chanzo, iliripoti taarifa ya Angel na mama yake mzazi kuhitaji msaada ikiwemo wa matibabu kutokana na hali ya afya yake iliyomsababisha kukatisha masomo. Kufuatia taarifa hiyo, alipatiwa msaada na kuanza matibabu Muhimbili hadi mauti yalipomkuta.

